Rais wa Marekani, Barack Obama anatua nchini kwa ziara ya siku mbili ikiwa ni hatua yake ya mwisho ya ziara yake barani Afrika.
Dar es Salaam. Yametimia! Baada ya siku kadhaa za kusubiri
kwa hamu, vitabu vya historia ya Tanzania vinaongezewa kumbukumbu wakati Rais wa
Marekani, Barack Obama atakapowasili nchini leo mchana kwa ziara ya siku mbili.
Ndege ya Air Force One itakayombeba Obama na msafara wake itakanyaga ardhi ya
Tanzania saa 8.40 mchana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
ambako atapokelewa na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete.
Obama ambaye anafuatana na mkewe Michelle na binti zake, Malia na Sasha,
anatua Tanzania ikiwa ni sehemu yake ya mwisho ya ziara yake barani
Afrika.
Anawasili Tanzania akitokea Afrika Kusini ambako alikwenda Ijumaa baada ya
ziara yake ya Senegal.
Historia imetimia
Imepita miaka 50, tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipotembelea
Marekani, Julai 13, 1963 na kukutana rais wa nchi hiyo wakati huo, John F
Kennedy na ziara hiyo inaaminika kuanzisha urafiki wa viongozi hao ambao umedumu
hadi sasa.
Ujio wa Rais Obama una maana na faida kubwa kwa Tanzania katika maeneo
ukiangalia kihistoria, kisiasa, kidiplomasia na kiuchumi pia.
Ziara ya Obama ni heshima kubwa kwa Tanzania na itaingia katika vitabu vya
kihistoria kwani ana rekodi ya kuwa mtu mweusi wa kwanza kuchaguliwa kuongoza
taifa la Marekani. Kuchaguliwa kwake (Obama), ambaye baba yake mzazi alikuwa na
asili ya Kenya kuliashiria nuru mpya kwa siasa za Marekani kwani watu weusi wa
taifa hilo kwa miaka mingi walikuwa wakipigania haki za kufaidika na fursa za
kiuchumi na kisiasa katika taifa la Marekani.
Tanzania, kwa miaka mingi ilikuwa inaunga mkono harakati za watu weusi na
ndiyo maana iliikuwa karibu na viongozi wa harakati za kupigania haki za watu
weusi.
Mwalimu Julius Nyerere alikuwa karibu na Martin Luther King na mkewe Correta
, ambao waliongoza harakati za mtu mweusi kujikomboa.Pia, viongozi wengine wa
harakati hizo za mtu mweusi kutambuliwa kule Marekani, Jesse Jackson, Andrew
Young na Malcolm X waliitembelea Tanzania mara nyingi. Obama alipochaguliwa
kushika nafasi hiyo mwaka 2008 alifurahiwa na wapenda amani kote duniani na hasa
Waafrika kwani walimhesabu kuwa ni sehemu yao.
Kuja kwake leo ni heshima kubwa kwani Tanzania inakuwa nchi ya nne Afrika
kutembelewa na Obama baada ya Ghana mwaka 2009 na ziara yake ya hivi karibuni ya
nchi za Senegal na Afrika Kusini.
Ukizingatia kuwa Obama ana miaka mitatu na nusu kabla ya kumaliza kipindi
chake cha pili cha uongozi wake huenda ziara hii ndiyo ikawa ya mwisho kwake
barani Afrika akiwa na wadhifa wa rais.