Wednesday, June 5, 2013

Ngwair kuagwa leo

 Dar es Salaam. ‘Alale pema peponi kamandaaa, alale pema peponi Mangweaaa’ Hayo ni maneno yaliyoimbwa na mamia ya vijana waliokuwa wanasukuma gari lililobeba mwili wa msanii Albert Mangweha, maarufu kama Ngwair.
Ngwair alifariki wiki iliyopita nchini Afrika Kusini alikokwenda kwa shughuli za muziki na mwili wake kuletwa jana mchana, Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam.
Simanzi ilitanda eneo zima la uwanja walikojazama mashabiki wa sanaa ya muziki, wengi wao wakiwa vijana wakati jeneza la Ngweair likitolewa sehemu ya ndani ya uwanja na kuletwa nje.
Vilio pia vilitawala kutoka kwa ndugu wa marehemu na watu wengine walioshindwa kuvumilia baada ya kushuhudia jeneza hilo likitolewa nje tayari kwa safari ya kupelekwa Hospitali ya Taifa, Muhimbili.
Kutokana na wingi wa watu, vijana wa skauti walilazimika kufanya kazi ya ziada kuunganisha mikono yao ili gari lililobeba mwili wa Mangwair liweze kupita bila kuzongwa, jambo lililowashinda
 nguvu.
Hali ilikuwa tofauti baada ya kundi la vijana kuendelea kuimba wimbo wa Kamanda, huku wakisukuma gari lililobeba mwili wa Ngwair na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.
Kadri mwili wa msanii huyo ulivyokuwa ukisogea mbele, ndivyo watu hasa vijana walivyokuwa wakijitokeza kutoka pembezoni mwa barabara na kuungana na wengine kusukuma gari.
Kazi ya kusukuma gari hiyo iliendelea kwa muda mrefu kupita barabara kuu ya Pugu kuelekea Muhimbili, ambako mwili wake ungehifadhiwa kabla ya kuagwa.
Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Ado Novemba alisema mwili wa marehemu utaagwa leo kwenye Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa sita mchana.
Baada ya hapo, marehemu atasafirishwa kwenda Morogoro kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika kwenye makaburi ya Kihonda.


No comments:

Post a Comment