Saturday, June 15, 2013

Upepo mkali waezua madarasa matano Rorya


Rorya. Upepo mkali umeezua vyumba vitano vya madarasa na ofisi moja ya walimu katika Shule ya Msingi Kogaja,Kata ya Ikoma katika Wilaya ya Rorya Mara.
Akitoa taarifa kwa Mbunge wa Jimbo la Rorya, Lameck Airo wakati alipotembelea na kuangalia maafa hayo,Afisa Mtendaji wa kijiji hicho,Lucas Ombonya alisema hata hivyo katika maafa hayo hakuna mtu yeyote ambaye alijeruhiwa kwa kuwa shule hiyo ilikuwa imefungwa kufuatia likizo ya mwezi wa sita.
Hata hivyo,Ombonya alisema tathmini ambayo ilifanywa na kamati ya maafa ya kijiji hicho ilibaini kuwa zinahitajika Sh9.2 milioni ili kurejesha majengo hayo katika hali yake ya kawaida.
Kwa upande wake,mbunge wa jimbo hilo alisema watahakikisha wanatatua tatizo hilo la maafa kwa shule hiyo na kulaani vitendo vya baadhi ya viongozi kuhamasisha ubaguzi wa itikadi za kisiasa kwa kile alichodai kuwa ni kuzorotesha maendeleo ya kijamii.
Mbunge huyo alitoa kiasi cha Sh3milioni kama mchango wake binafsi kwa ajili ya kuboresha shule hiyo,huku akiwataka na wengine walioguswa na maafa hayo kuchangia.
Naye Mwenyekiti wa CCM Rorya,Samwel Kiboye,kabla ya kutoa mchango wake wa Sh1milioni aliwataka wananchi kuepuka vurugu wakati wa kutoa maoni yao ya kuchangia rasimu ya katiba ili kuwezesha kupata maoni ambayo yatawezesha taifa kupata katiba nzuri.
Katika ziara hiyo ya kukagua maafa hayo,mbunge huyo ameitisha harambee ya papo kwa papo ambapo kiasi cha Sh9milioni kilichokuwa kinahitajika kilipatikana,huku Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rorya, Chaeles Ochere,akichangia Sh1.2 milioni,Halmashauri Sh1.5milioni, huku wananchi wa kijiji hichona diwani wao wakichangia Sh2milioni.

No comments:

Post a Comment