Thursday, June 6, 2013

‘Chamber Squad’

BAADA ya ‘sintofahamu’ na taharuki iliyowakumba wanamuziki hasa kundi la Chamber Squad baada ya kifo cha msanii mwenzao, Albert Mangwea ‘Ngwair,’ swahiba wake, Mez B, anatoa wasifu wa ‘Ngwair’ kama ifuatavyo:
“Tunasema asante Mungu kupata nafasi hii kusema machache kuhusu ndugu yetu Albert Mangwea ‘Ngwair’ ‘Cow Obama.’
Sisi kama Chamber Squad, tungependa kumzungumzia zaidi kama ‘Ngwair’ na si kama Albert, maana tayari ameshazungumziwa katika risala nyingi,” hivi ndivyo anavyoanza kusema Mez B.
Anasema: “Kwa kifupi, Ngwair tulikutana kwa mara ya kwanza Shule ya Sekondari ya wavulana Mazengo iliyopo mkoani Dodoma mwaka 1997 wakati huo akiwa kidato cha kwanza.
“Kipindi hicho tulikutana na kaka zetu ambao ni Augustino Makale a.k.a Tino na Athumani Kabongo a.k.a. Dark Master. Hawa ndio waasisi wa Chamber Squad pamoja na kaka zetu, Alkapaono, G2 The Bye na Mussa Gama.”
Maana halisi ya Chamber Squad
“Ni vyumba vya kusomea ambavyo kaka zetu hawa walikuwa wanakesha humo wakijisomea usiku kucha na wanapochoka, ndipo redio zinawashwa na ‘Freestyle’ zinaanza kupooza.
“Tulihamasika na ‘style’ yao , ndipo sisi pia tukaunda kundi dogo lililojulikana kwa jina la ‘Chamber Flavor Guys (C.F.G) lililoundwa na mimi ‘QG’, ambaye kwa sasa nafahamika kama Mez B, Mangwea na Malo Star, ambaye kwa sasa hafanyi kazi ya muziki.”
Asili ya jina la Ngwair
Mez B anasema jina la ‘Ngwair’ halikutokea hewani tu, lilitokana na jina lake halisi la Mangwea, ambapo wakati wanasoma Mazengo, walikuwa na kawaida ya kucheza mpira wa kikapu hadi usiku wa manane.
“Hiyo ikatufanya tumuite ‘Man In The Air’ kutokana na ukali wake wa kupiga ‘free throws’ ndipo jina la Mangwair lilipozaliwa mpaka kuwa ‘Ngwair’,” anasema Mez B.
“Mwaka uliofuata (1998), tulitoa albamu yetu ya kwanza iliyofahamika kwa jina la ‘Heshima kwa Wote’, tulirekodi chini ya mtayarishaji Xpela katika Studio ya Tushikamane iliyopo mkoani Morogoro ambayo ilisambazwa na Wananchi Store.
Baada ya kuhitimu elimu yetu ya sekondari, tuliamua kama ‘Chamber Flavor Guys’ kuwa chamber rasmi na kujiunga na Dark Master, hapo pia akaingia Noorah na Tony, ambapo maskani yetu yalikuwa Kijitonyama kwenye makazi ya Tony.
“ Tuliweza kutengeneza nyimbo kama ‘Ahadi za Boss’, ‘Party East Zoo’ na Shega Tuu’, ndipo mwenzetu alipoweza kupata nafasi ya kurekodi ‘Gheto Langu’ ndani ya Studio ya Bongo Records ikiwa chini ya P. Funk ‘Majani.’
“Baada ya hapo, alitoa albamu yake ya kwanza ya ‘a.k.a. Mimi,’ chini ya usimamizi wa DJ Venture ambayo ilisababisha kushinda tuzo mbili za muziki za Kilimanjaro Music Awards ambazo ni albamu bora ya Hip Hop na wimbo bora wa kushirikiana,” anasema.
Huu ndio ukawa mwanzo wa kutoa ‘hit’ baada ya ‘hit’ ya nyimbo nyingi ambazo ni ‘Kama Vipi’ ya Mez B’, ‘Ice Cream’ ya Noorah na nyingine nyingi pamoja na kufanya maonesho kadhaa.
“Rafiki yetu alikuwa mtu mchangamfu na mwenye vituko sana, huwezi kukaa naye bila kucheka. Na uwezo wake wa kukariri nyimbo na uthubutu wa kila jambo vilikuwa ni vitu tofauti sana kulingana na umri wake siku zote za uhai wake,” anasema Mez B.
Ngwair na umeneja wa klabu
“Nakumbuka wakati tuko kidato cha nne, Ngwair alikuwa tayari ni Meneja wa Club ya La Azizi iliyopo Dodoma, tukienda jioni tunakuta mwenzetu ameshika kipaza sauti ‘Mic’ anaimbisha jukwaani na wachezaji ‘dancers’ tukianzia kuelezea vituko tulivyopitia tutatumia hata siku nzima, lakini havitaisha na kuchekesha.
“Tunawashukuru Watanzania kujitokeza kwa wingi, hii inaonesha jinsi gani upendo mlionao kwa ndugu yetu. Mimi Mez B, Dark Master, Noorah na close friends wake Ben Mshua, Thuwein na Pius tunaahidi tutaendeleza alichokiacha njiani, tunaomba mwendelee kutuonesha upendo huu na ushirikiano wenu,” anasema Mez B.
Mangwair aliyefariki dunia Mei 28 nchini Afrika Kusini na kuzikwa Juni 6, nyumbani kwao Kihonda, mkoani Morogoro, kwa hakika ameondoka huku mchango wake kwenye ‘gemu’ na taifa kwa ujumla ukiwa bado unahitajika.
Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya Mangwair. Amina.

1 comment: